2 Samuel 1:2-16

2 aSiku ya tatu akaja mtu mwenye nguo zilizoraruka na mavumbi kichwani mwake kutoka kwenye kambi ya Sauli. Alipomjia Daudi, akajitupa chini ili kumpa heshima.

3Daudi akamuuliza, “Wewe umetoka wapi?”

Akamjibu, “Nimetoroka kutoka kambi ya Waisraeli.”

4 bDaudi akamuuliza, “Ni nini kilichotokea? Niambie.”

Akasema, “Watu walikimbia kutoka vitani. Wengi wao walianguka na kufa. Naye Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa.”

5Ndipo Daudi akamwambia huyo kijana aliyemletea taarifa, “Je, umefahamuje kwamba Sauli na Yonathani mwanawe wamekufa?”

6 cYule kijana akasema, “Nilijipata huko Mlima Gilboa, naye Sauli alikuwa huko akiegemea mkuki wake, na magari ya vita na wapanda farasi wa upande wa adui wakawa wamemkaribia sana. 7Alipogeuka na kuniona, akaniita, nami nikasema, ‘Je, nifanye nini?’

8 d“Akaniuliza, ‘Wewe ni nani?’

“Nikamjibu, ‘Mimi ni Mwamaleki.’

9 e“Kisha akaniambia, ‘Nikaribie mimi na uniue! Niko katika maumivu makali ya kifo, lakini bado ningali hai.’

10 f“Kwa hiyo nikamkaribia nikamuua, kwa sababu nilijua kwamba baada ya kuanguka hangeweza kupona. Nami nikachukua lile taji lililokuwa kichwani mwake na utepe uliokuwa mkononi mwake nami nimevileta hapa kwa bwana wangu.”

11 gNdipo Daudi pamoja na watu wote waliokuwa pamoja naye wakazishika nguo zao na kuzirarua. 12Wakaomboleza, wakalia pia na kufunga mpaka jioni kwa ajili ya Sauli na Yonathani mwanawe, kwa ajili ya jeshi la Bwana na nyumba ya Israeli, kwa sababu wameanguka kwa upanga.

13 hDaudi akamwambia yule kijana aliyemletea taarifa, “Wewe ni mwenyeji wa wapi?”

Akamjibu, “Mimi ni mwana wa mgeni, Mwamaleki.”

14 iDaudi akamuuliza, “Kwa nini hukuogopa kuinua mkono wako ili kumwangamiza mpakwa mafuta wa Bwana?”

15 jKisha Daudi akamwita mmoja wa watu wake na kumwambia, “Nenda ukamuue!” Kwa hiyo akampiga, naye akafa. 16 kKwa maana Daudi alikuwa amemwambia, “Damu yako iwe juu ya kichwa chako mwenyewe. Kinywa chako mwenyewe kimeshuhudia dhidi yako uliposema, ‘Nilimuua mpakwa mafuta wa Bwana.’ ”

Copyright information for SwhNEN